SIMBA YAFUATA KIUNGO COLOMBIA NA URUGUAY


Uongozi wa Klabu ya Simba, chini ya Kaimu Rais, Salim Abdallah ‘Try Again’, unaendelea na mchakato wa kuimarisha kikosi chao ambapo upo kwenye mchakato wa kwenda kusaka kiungo matata katika nchi za Amerika Kusini. Simba ambayo jana iliwatangaza kipa Deogratius Munish ‘Dida’, beki Pascal Wawa na mshambuliaji Meddie Kagere, imesema sasa ni zamu ya kuimarisha nafasi ya kiungo. Katika nchi za Amerika Kusini ambazo Simba imepanga kwenda kumchukua kiungo huyo matata ni Chile, Colombia na Uruguay.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba, kimelieleza Championi Ijumaa kuwa, usajili wa kiungo huyo utafanywa kwa umakini mkubwa kwani baada ya kuimarisha sehemu nyingine, sasa ni zamu ya nafasi hiyo kuongezewa nguvu. “Usajili kwetu haujamalizika, kama unavyojua kwenye timu kuna sehemu ile za kati lazima iwe imara ambayo huitwa uti wa mgongo.

“Tumefanya marekebisho kwenye nafasi ya kipa, beki wa kati na mshambuliaji, sasa ni zamu ya kiungo wa kati. “Kiungo huyo tumepanga kwenda kumchukua huko Amerika Kusini kwenye nchi za Colombia, Uruguay na Chile, siyo utani, tumedhamiria kufanya kweli kwa sababu tuna mashindano makubwa yanatusubiri, hivyo lazima tuwe imara,” kilisema chanzo hicho.

Wakati huohuo, mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi raia wa Uganda, amepewa mapumziko maalum na klabu hiyo ili apone kabisa majeraha ya enka yanayomsumbua. Okwi ambaye msimu uliomalizika hivi karibuni aliibuka kuwa Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Bara akifunga mabao 20 na kuisaidia Simba kutwaa ubingwa wa ligi hiyo, aliondoka nchini siku chache kabla ya timu yake haijacheza mechi ya mwisho ya msimu dhidi ya Majimaji.

Licha ya kuukosa mchezo huo, pia Okwi alishindwa kuwepo kwenye kikosi cha Simba kilichoshiriki michuano ya SportPesa Super Cup iliyofanyika nchini Kenya hivi karibuni ambapo timu hiyo ilimaliza nafasi ya pili, huku pia akiikosa michuano ya Kagame inayoanza leo Ijumaa.

Taarifa kutoka katika benchi la ufundi la Simba ambalo kwa sasa lipo chini ya Mrundi, Masoud Djuma, zinasema kuwa, mchezaji huyo yupo nchini kwao Uganda akiendelea kuuguza majeraha hayo na wanatarajia kuwa naye tena msimu mpya ukianza Agosti, mwaka huu.

“Sababu za Okwi kutoungana na wenzake kwa muda mrefu zinatokana na kupewa mapumziko maalum kwa sababu aliondoka akiwa majeruhi, hivyo tukaamua kumpa mapumziko hayo hadi apone kabisa.

“Kipindi kile wakati anacheza ligi, alikuwa akicheza akiwa na majeraha lakini tulilazimika kumchoma sindano za kupunguza maumivu ili aweze kuipambania timu hadi ilipofanikiwa kutwaa ubingwa, tukampa mapumziko hayo,” alisema mtu huyo.

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post