CHIRWA ATAJA ANAPOTAKIWA KWENDA


Mshambuliaji mahiri wa Yanga, Obrey Chirwa.
LICHA ya kuendelea kutajwa kuwa anaweza kutua katika kikosi cha Simba au Azam FC, mshambuliaji mahiri wa Yanga, Obrey Chirwa, amefunguka kuwa tayari ana ofa nyingi kutoka barani Ulaya.
Chirwa alijiunga na Yanga msimu uliopita akitokea FC Platinum ya Zimbabwe na huu ukiwa ni msimu wake wa pili ndani ya klabu hiyo ambayo msimu huu imeshindwa kutetea ubingwa wake wa Ligi Kuu Bara.
Straika huyo raia wa Zambia amekuwa akitajwa kuwaniwa na klabu tofauti za hapa nchini na hii ni baada ya mkataba wake kumalizika msimu huu ndani ya klabu hiyo.
Akizungumza straika huyo alisema kuwa kwa sasa ana ofa nyingi, nyingine ni za kutoka nje lakini hawezi kuziweka hadharani kwa sasa.
Straika huyo alisema hawezi kusema kwa sasa msimu ujao atakuwa wapi ila watu watajua baadaye pale mambo yake yatakapokuwa yamekamilika.
“Siwezi kusema kama nabaki Yanga au nitaondoka, hiyo siyo kazi yenu ila wewe fahamu tu kwamba mimi nina ofa nyingi sana kwa sasa kuna timu hadi za Ulaya zinanitaka lakini siwezi kukwambia ni timu gani, sababu siyo jukumu lako kujua,” alisema Chirwa.
Msimu huu mshambuliaji huyo amefanikiwa kufunga mabao 12 na msimu wake wa kwanza alifanikiwa kufunga mabao 12 pia.

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post