Golikipa mkongwe wa Misri Essam El Hadary amesema watafanya uamuzi kwa pamoja
Nahodha wa timu ya taifa ya Misri ambaye pia ndiye mlinda lango wao Essam El Hadary amesema wachezaji wa taifa hilo wataamua kwa pamoja kuhusu kufunga wakati wa mwezi huu mtukufu wa Ramadhan.
Hii ni kwa sababu mfungo huo wa Ramadhan wakati huu umelingana na wakati ambao mataifa yanajiandaa kwa michuano ya Kombe la Dunia ambalo litaanza 14 Juni nchini Urusi.
Wachezaji wanahitajika kuwa kambini wakijiandaa na kucheza mechi za kirafiki.
Ramadhan, mwezi ambao Waislamu hula hawali chakula wala kunywa maji kuanzia macheo hadi machweo, ulianza 16 Mei na unatarajiwa kumalizika michuano ya Kombe la Dunia ikianza, karibu na 15 Juni.
"Tutafanya mkutano kama wachezaji siku chache zijazo na kisha tutawafahamisha wakufunzi kuhusu uamuzi wetu," alisema El Hadary, 45.
Mabingwa hao mara saba wa Afrika watacheza na Kuwait wikendi hii mechi ya kirafiki kabla ya mechi dhidi ya Colombia na Ubelgiji.
Kisha, wataanza kampeni yao Kombe la Dunia Kundi A mnamo 15 Juni dhidi ya uruguay, na baadaye dhidi ya wenyeji Urusi na kisha Saudi Arabia.
Mkurugenzi wa timu Ihab Leheta ameeleza kuwa wakufunzi hawataingilia kati uamuzi wa wachezaji.
"Kufunga ni uamuzi wa wachezaji, iwapo wanataka kufanya hivyo, wakufunzi hawawezi kuwalaumu, hebu tusubiri tuone wachezaji wataamua nini," amesema.
Mkufunzi kuu wa timu ya taifa kutoka Argentina Hector Cuper anafahamu uzito wa suala hilo.
"Mfungo ndilo jambo muhimu zaidi kwa sasa, nina wasiwasi kwamba unaweza kuwaathiri wachezaji katika Kombe la Dunia," alisema.
Chimbuko la Mo Salah, Firauni nguzo ya Liverpool
"Sifikiri kwamba kusafiri wakati wa mechi za kirafiki kutawachosha, ninawaandaa tu vyema kwa ajili ya mechi hizo."
Iwapo wachezaji hao wataamua kufunga, Cuper amefanya maandalizi ya kuwapa wataalamu wa kuwapangia jinsi ya kula na kulala na kuheshimu matakwa ya mfungo wa mwezi wa Ramadhan.