TFF YAMUOMBA JAMBO HILI RAIS MAGUFULI


Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia amefunguka na kudai atalifanyia kazi kwa vitendo agizo lililotolewa kwenye sherehe za kukabidhi vikombe vya ushindi hivi karibuni uwanja wa Taifa na Rais Dkt. Magufuli ili waweze kuitendea haki tasnia ya michezo.

Karia amesema hayo kwenye taarifa yake iliyotolewa na Afisa Habari na Mawasiliano ya TFF, Cliford Mario Ndimbo yenye lengo la kumshukuru Rais Dkt. Magufuli kwa kuweza kushiriki sherehe za kukabidhi kombe la mshindi wa pili kwa watoto wanaoishi mazingira magumu, Ubingwa wa Cecafa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kukabidhi Kombe la Ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara zilizofanyika mwishoni mwa juma lililoisha.

"Kwa namna ya kipekee kwa niaba ya TFF napenda kumshukuru Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kukubali ombi letu la kuwa mgeni rasmi katika tukio hilo. Tumefarijika kwa Rais Magufuli kuungana na wanamichezo na kuzungumza nao, alichokizungumza tumekipokea na tunaahidi tutakifanyia kazi kwa vitendo katika kuunga mkono jitihada zake za dhati kuona mpira wa miguu unapiga hatua", amesema Karia.

Pamoja na hayo, Karia ameendelea kwa kusema "tunaamini wanamichezo wengine nao wataunga mkono jitihada hizo za Rais wa Tanzania na jitihada za TFF ili kufanikisha lengo. TFF tutahakikisha tunasimamia mpira wa Tanzania kwa kuongozwa na sheria, kanuni na utaratibu na hatutakubali kuona mtu anakwenda kinyume na kutaka kuvuruga taswira nzuri ya mpira tuliyoanza kuijenga katika kipindi kifupi tulichoingia madarakani".

Aidha, Karia amesema anaamini ushirikiano wao na serikali ya awamu ya tano iliyopo chini ya Rais Magufuli utafikia lengo kwa pamoja.

"Serikali ya awamu ya tano imekuwa na ushirikiano mkubwa na TFF katika kufanikisha masuala mbalimbali ushirikiano ambao hakika utaleta matunda zaidi. Tunaamini kuwa timu zetu za Taifa zitafanya vizuri kama ambavyo timu yetu ya Vijana U-17 Serengeti Boys ilivyofanya vizuri na kuchukua kombe nchini Burundi na timu ya wasichana ya kituo cha TSC nao walivyofanya vizuri na kufika fainali kombe la dunia la watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu. Hakika ni mfano wa kuigwa mpaka kwenye ngazi ya klabu kwa kushinda mataji mbalimbali.", amesisitiza Karia.

Kwa upande mwingine, Karia amemuhakikishia Rais Magufuli kuendelea kusimamia mpira wa Tanzania ipasavyo kwa kushirikiana na serikali kwenye kila eneo ambalo linalohitajika msaada wa serikali. 

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post