Hatma ya Majimaji kubaki ligi kuu Tanzania bara itaamua leo jioni kwenye mechi yao dhidi ya mabingwa wapya wa msimu huu Simba SC.
Licha ya mashabiki kuonekana kukata tamaa na timu yao na wakiwa tayari kwa lolote, kocha msaidizi wa Majimaji FC Habib Kondo amesema kufanya vibaya kwa timu yao kumesababishwa na viongozi wa timu yao.
“Uchumi ndio umepelekea Majimaji kuwa hapa ilipo, viongozi inabidi wajitathmini kwa nini timu imefika hapa. Mwazo wa ligi hadi mwisho wa ligi viongozi hawana maelewano mazuri na wachezaji, kila siku wachezaji wanadai tangu tumeanza ligi hadi tunamaliza.”
“Wanasongea tunawashukuru sana wametu-support kipindi chote tulipokuwa tukifanya vibaya kwa hiyo ‘no comment’ kwao.”
Kondo pia ameonesha wazi kukata tamaa: “Majimaji kubaki ligi kuu ni sawa na Tembo kupenya tundu la sindano.”
Mechi kati ya Majimaji dhidi ya Simba itaamua hatma ya Majimaji kusalia VPL au kushuka daraja lakini wanategemea matokeo ya mchezo wa Ndanda vs Stand United.