Mshambuliaji wa Chelsea Alvaro
Morata ameachwa nje ya kikosi cha wachezaji 23 watakaowakilisha
Uhispania katika michuano ya Kombe la Dunia nchini Urusi.
Mchezaji
huyo wa miaka 25 alifunga mabao 11 msimu wake wa kwanza Stamford Bridge
na alichezeshwa kama nguvu mpya dakika za mwisho mwisho wakati wa
fainali ya Kombe la FA ambapo Blues walilaza Manchester United 1-0
Jumamosi.Wachezaji wenzake Morata katika Chelsea Marcos Alonso na Cesc Fabregas wanaungana na beki wa Arsenal Hector Bellerin katika kuachwa nje ya kikosi.
Mtangulizi wa Morata katika Chelsea Diego Costa ni miongoni mwa washambuliaji watakaoelekea Urusi.
Julen Lopetegui amewaweka wachezaji wanne wa Ligi ya Premia kwenye kikosi chake: David De Gea, David Silva, Cesar Azpilicueta na Nacho Monreal.
Uhispania wataanza kampeni yao Urusi kwa mechi dhidi ya Ureno mnamo 15 Juni mjini Sochi.
Morata aliwachezea mabingwa hao wa dunia wa 2010 mara ya mwisho Novemba 2017 alipofunga katika mechi ambayo walishinda 5-0 dhidi ya Costa Rica.
Licha ya kuachwa nje ya kikosi, mshambuliaji huyo ameandika kwenye Twitter ujumbe wa kuwapongeza na kuwatakia heri wenzake katika michuano hiyo.
Real Madrid na Barcelona wametoa wachezaji 10 kwenye kikosi hicho, ikiwa ni pamoja na kigogo wa Barca Andres Iniesta ambaye aliwachezea miamba hao wa Catalonia mechi yake ya mwisho Jumapili.
Kikosi kamili cha Uhispania
Walinda lango: David de Gea (Manchester United), Pepe Reina (Napoli), Kepa Arrizabalaga (Athletic Bilbao).Mabeki: Jordi Alba (Barcelona), Nacho Monreal (Arsenal), Alvaro Odriozola (Real Sociedad), Nacho Fernandez (Real Madrid), Dani Carvajal (Real Madrid), Gerard Pique (Barcelona), Sergio Ramos (Real Madrid), Cesar Azpilicueta (Chelsea).
Kiungo wa kati: Sergio Busquets (Barcelona), Isco (Real Madrid), Thiago Alcantara (Bayern Munich), David Silva (Manchester City), Andres Iniesta (Barcelona), Saul Niguez (Atletico Madrid), Koke (Atletico Madrid).
Washambuliaji: Marco Asensio (Real Madrid), Iago Aspas (Celta Vigo), Diego Costa (Atletico Madrid), Rodrigo Moreno (Valencia), Lucas Vazquez (Real Madrid).
Tags
KOMBE LA DUNIA 2018