KAMUSOKO ATUPIA 1, YANGA IKIIUA MBAO FC UWANJA WA TAIFA


Mabingwa wa kihistoria wa soka Tanzania, Yanga leo wamefanikiwa kuondoka na alama zote tatu uwanja wa Taifa baada ya kuilaza Mbao FC bao 1-0 kwenye mchezo wa ligi kuu ya Vodacom.

Kabla ya mchezo huo Yanga ilikuwa imecheza michezo tisa bila ya kupata ushindi tangu kuondoka kwa aliyekuwa kocha wake George Lwandamina.

Lakini dalili za kuondoka na alama zote tatu leo zilionekana mapema baada ya Yanga kuanza mchezo huo kwa kasi na kukosa mabao ya mapema kupitia kwa Yusuph Mhilu na Pius Buswita.

Bao pekee la Yanga lilifungwa na nahodha Thabani Kamusoko kwenye dakika ya 25 kupitia mpira wa adhabu aliopiga nje kidogo ya 18 na kuujaza moja kwa moja wavuni.

Yanga yakataa uteja mbele ya MBAO yaidungua bao 1-0

A post shared by Jmartine WaTz (@jmartinemedia) on May 22, 2018 at 8:52am PDT


Mbao FC haikuwa na mchezo mzuri kwenye kipindi cha kwanza kutokana na kuzidiwa hasa sehemu ya kiungo lakini ilirejea imara kwenye kipindi cha pili.

Lakini ni Yanga iliyokosa nafasi za wazi zaidi katika kipindi hicho kupitia kwa Matheo Antony aliyeingia kuchukua nafasi ya Mhilu na Geofrey Mwashiuya.

Mwashiuya alikosa nafasi ya wazi baada ya kushindwa kupasia wavuni krosi ya Matheo aliyekuwa akiisumbua safu ya ulinzi ya Mbao FC.

May 25 Yanga itacheza mchezo wake wa mwisho wa kiporo dhidi ya Ruvu Shooting kwenye uwanja wa Taifa kabla ya kumaliza msimu kwa kuchuana na Azam FC May 28 kwenye uwanja huo huo.

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post