Mbunge Jimbo la Kawe kupitia tiketi ya CHADEMA, Halima Mdee amekamatwa na Jeshi la Polisi leo asubuhi kwenye uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Jijini Dar es Salaam akiwa anatokea nchini Afrika Kusini kwaajili ya kupatiwa matitabu.
Hayo yamethibitishwa na Mbunge wa Jimbo la Ubungo kupitia Chadema Saed Kubenea na kusema ni kweli Halima Mdee amekamatwa leo na Jeshi la Polisi kutokana na yeye kutoripoti katika kesi iliyofunguliwa japokuwa alitoa taarifa ya udhuru.
"Ni kweli Halima Mdee amekamatwa leo asubuhi akiwa Airport Jijini Dar es Salaam na Jeshi la Polisi, inafahamika kuwa Mdee ni miongoni mwa viongozi wa Chadema wanaoshtakiwa kwenye kesi ambayo ipo Mahakamani ambapo Mwenyekiti Freeman Mbowe akiwa mmoja wao", amesema Kubenea.
Pamoja na hayo, Kubenea ameendelea kwa kusema "walikuwa nje kwa dhamana kabla ya kesi kupelekwa Mahakamani, kwa hiyo Halima alikuwa hajaenda kuripoti Polisi siku waliyoambiwa waende kuripoti Polisi kwa maana yeye alikuwa nje ya nchi. Sasa amerejea nchini leo asubuhi ndipo walipomkamata Airport".
Kwa upande mwingine, Kubenea amesema kukamatwa kwa Halima Mdee bila shaka Jeshi la Polisi linataka kumuunganisha na viongozi wengine waliokuwa gerezani mpaka muda huu lisha ya kwamba wamepatiwa dhamana ya Mahakama.