Nahodha wa Yanga Nadir Haroub ‘Cannavaro’ amewaambia wanachama na wapenzi wa Yanga wasife moyo baada ya timu yao kutolewa na Singida United kwenye mashindano ya Azam Sports Federation Cup.
“Tunamsukuru Mungu tumefika salama Morogoro, tunawaomba mashabiki wa Yanga wasife moyo kutokana na kupoteza mchezo wetu dhidi ya Singida United japo tulijitahidi lakini tukafungwa kwa penati.”
“Tuna mechi ya kimataifa siku ya Jumamosi, tunaomba mashabiki waje kwa wingi kutupa sapoti ili tuweze kufanya vizuri.”
“Nafasi ya ubingwa wa ligi bado ipo kwa sababu sisi na Simba tuna pointi sawa lakini tumewazidi kwa mchezo mmoja, kwa upande wetu bado tuna nafasi ya kuwa mabingwa na bado tuna nafasi ya kuingia hatua ya makundi ya kombe la shirikisho Afrika.
Kwa sasa Yanga imeweka kambi mjini Morogoro kwa ajili ya maandalizi kuelekea mchezo wao wa kimataifa dhidi ya waethiopia, Yanga ilipoteza nafasi ya kuiwakilisha Tanzania katika michuano hiyo hivyo nafasi iliyobaki kwao ni kutwaa ubingwa wa ligi ili kuwa wawakilishi katika mashindano ya vilabu bingwa Afrika.
Nafasi ya kuwakilisha Tanzania bara katika mashindano ya kombe la shirikisho Afrika ipo mikononi mwa timu nne zilizofuzu hatua ya nusu fainali ya ASFC ambazo ni stand united, JKT Tanzania, Mtibwa Sugar na Singida United.