Ureno 0-3 Uholanzi: Cristiano Ronaldo apigwa breki mjini Geneva


Cristiano RonaldoHaki miliki ya pichaEPA
Mabingwa wa Ulaya Ureno walipokezwa kichapo cha kushangaza na Uholanzi katika mechi ya kimataifa ya kirafiki iliyochezewa mjini Geneva, Uswizi.
Winga wa zamani wa Manchester United Memphis Depay na mshambuliaji wa zamani wa Liverpool Ryan Babel waliwaweka Waholanzi 2-0 mbele.
Beki wa Uholanzi Virgil van Dijk, ambaye majuzi alitawazwa nahodha mpya wa timu hiyo, alifunga la tatu.
Mchezaji wa Ureno Joao Cancelo alipewa kadi nyekundu dakika ya 61 baada ya kupokezwa kadi ya pili ya manjano.
Cristiano RonaldoHaki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Image captionCristiano Ronaldo alikuwa amefunga mabao mechi nane mfululizo kabla ya mechi hiyo
Katika mechi hiyo, mkimbio wa kufunga mechi nane mtawalia wa mshambuliaji nyota wa Ureno anayechezea Real Madrid Cristiano Ronaldo ulifikishwa kikomo.
Nahodha huyo wa Ureno aliondolewa uwanjani dakika ya 68 na nafasi yake akaingia kiungo wa Monaco Joao Moutinho.
Ronaldo alikuwa amefunga mabao 17 akichezea Real na mawili akichezea Ureno dhidi ya Misri Ijumaa katika kipindi hicho alichofunga mabao mechi nane mtawalia.
Kundi B
Ureno wamo Kundi B katika Kombe la Dunia pamoja na Uhispania, Morocco na Iran.
Lakini Uholanzi, ambao walishindwa 1-0 na England mechi ya kwanza Ronald Koeman akiwa mkufunzi wao, hawakufuzu kwa michuano hiyo itakayoanza mwezi Juni.

Messi kurejea dimbani

Kwingineko, Lionel Messi anapangiwa kurejea uwanjani kuwachezea Argentina mechi ya kirafiki dhidi ya Uhispania Jumanne.
Hakucheza mechi ambayo walilaza Italia 2-0 mjini Manchester Ijumaa kutokana na jeraha la misuli, lakini ameimarika na kuruhusiwa kuchezea taifa lake mjini Madrid.
Kocha wa Argentina Jorge Sampaoli amesema Messi alifanya mazoezi kama kawaida Jumatatu.
Argentina's Lionel Messi and Sergio AgueroHaki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Image captionLionel Messi amepona jeraha la misuli lakini mwenzake Sergio Aguero bado hawezi kucheza
Nyota huyo wa Argentina huenda akacheza dhidi ya wenzake wa Barcelona wanaochezea timu ya Uhispania Gerard Pique na Jordi Alba.
Uhispania walitoka sare 1-1 na Ujerumani mjini Dusseldorf Ijumaa, na kuendeleza mkimbio wao wa kutoshindwa chini ya Julen Lopetegui hadi mechi 17.

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post