Brazil kukutana na Ujerumani kwa mara ya kwanza hii leo tangu 7-1


Ilikuwa ni July 8 mwaka 2014 wakati Thomas Muller akifunga bao la kwanza dakika ya 11, mimi na wapenda soka wote ulimwenguni tuliamini ni mechi ngumu, hata wakati Miroslav Klose akifunga la pili bado ilionekana inaweza kuwa ngumu.
Bao la 3 la Toni Kroos watu waliangaliana na kuguna na kabla mguno hujaisha sekunde zisizozidi 120 baadae Kroos alifunga tena na kila mtu akaona jambo baya linawatokea Brazil, ni kweli waliabika kwani ziliongezwa 3 nyingine wkafa bao 7 kwa 1 nyumbani kwao.
Hili lilikuwa tukio lililowavua Wabrazil nguo, ni tukio baya sana kwa Wabrazil kuliona na kizazi chao kinakua wakimuangalia Mjerumani kama adui wao mkubwa katika soka duniani kwa sasa kutokana na alichiwafanya siku zile.
Siku zimepita na mengi yakawasahaulisha lakini hii leo kwa mara ya kwanza tangu Brazil aaibishwe kwa kipigo kile cha mbwa mwizi wanakutana tena na Wajerumani na Wajerumani wanaonekana ni wanyama vile vile walivyowaacha 2014.
Ni ngumu kwa Ujerumani hii kuifunga 7, imekamilika kila eneo na hata ukifunga nao watakufunga lakini Brazil wanaweza kulipa kisasi kwa nia nyingine, wanaweza kulipa kisasi kwa kile ambacho Wahispania wameshindwa kufanya.
Ujerumani wana michezo 21 hakuna timu ambayo imewahi kuwafunga, mchezo wao dhidi ya Brazil katika uwanja wao wa nyumbani inaweza kuwapa nafasi Wabrazil kuwaonesha kile ambacho wengine wameshindwa kwa kuisimamisha rekodi yao.
Kwa nyakati tofauti Thiago Silva pamoja na kocha wake Tite wametaka mchezo huu usihusishwe na kisasi kwani kwa vyovyote vile hawawezi kubadili kile ambacho kilitokea mwaka 2014 na kusisitiza kwamba huu ni mchezo wa kirafiki tu.
Rekodi zinaonesha kwa ujumla Brazil amemfunga Ujerumani mara 12(tangu Ujerumani ikiwa West na East) huku Ujerumani akimfunga Brazil mara 5 na timu hizo mbili zikienda suluhu mara 5 katika jumla ya michezo 22 waliyokutana

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post