Mwandishi afunguka kilichomkimbiza Tanzania, Serikali yabeza shutma zake


Picha ya Ansbert Ngurumo akiwa FinlandHaki miliki ya pichaTWITTER/@NGURUMO
Image captionPicha ya Ansbert Ngurumo akiwa Finland
Mwandishi wa habari mwandamizi Ansbert Ngurumo ambaye amekimbilia ulaya nchini Finland kwa kile anachokiita kuwa ni kunusuru maisha yake, amezungumza na BBC.
Ngurumo ambaye amefanya kazi na vyombo kadhaa vya habari nchini Tanzania ikiwa ni pamoja na gazeti la Mwanahalisi ambalo limefungiwa hivi karibuni, anaishutumu serikali kwa kupanga njama hizo za kutoa uhai wake.
Lakini Msemaji wa serikali amepuuza madai hayo ya Bwana Ngurumo na kusema Ngurumo amekimbia kwa sababu zake binafsi na kwamba uhuru wa habari na kujieleza nchini Tanzania ni wa uhakika.
Aliyefanya mahojiano na wote hawa ni mwandishi wa BBC, Sammy Awami na haya ndio mazungumzo yao:
Presentational grey line
Sammy: Hii ni mara ya kwanza kwa mwandishi wa habari wa Tanzania, kukimbia nchi yake na kudai kuomba hifadhi katika nchi nyingine kwa madai ya kuwa hatarini kutokana na kazi yake ya uandishi wa habari.
Ngurumo: Kimsingi yaliyonikuta ni marefu sana lakini la msingi ni kuwa nimekimbia, nimejificha najihadhari na ni tofauti na wanaosema nimeikimbia nchi, mimi sijaikimbia nchi, nchi ni ya kwangu, mimi ni mtanzania na najua mambo haya yataisha na nitarudi. Lakini kitu kikubwa ni kwamba nimewakimbia wauwaji, nimekimbia watesaji , nimekimbia watu wanaowateka watu ambao wanalindwa na dola..
Sammy:Umetoa shutuma kwamba hawa watekaji, wanaoua watu, wanalindwa na dola, hizi ni shutuma nzito sana Bwana Ngurumo, una uthibitisho gani kuwa dola inawalinda hawa watu?
Ngurumo: Kama hutaki kuituhumu dola katika mazingira haya, unamtuhumu nani ambaye anapaswa kushughulikia haya? Amepotezwa Azory mwandishi habari wa Mwananchi, waajiri wake na wafanyakazi wenzake wameandamana wametaka arudi. Leo ni zaidi ya siku 100 hajulikani alipo, serikali iliyohai inayofanya kazi, inayolinda uhuru wa raia, haitoi majibu nani atuhumiwe kama si wao?
Ansbert NgurumoHaki miliki ya pichaNGURUMO
Image captionAnsbert Ngurumo alikuwa akiandikia gazeti la MwanaHalisi
Sammy: Lakini serikali inasema inaendelea na uchunguzi wa matukio yote haya,kwa nini usiiamini?
Ngurumo: Vitendo na mwenendo na tabia yake vinaifanya isiaminike, kwa sababu hatuoni ikichunguza. Kama serikali inaweza kukamata watu wanaoikosoa haraka, ikawapeleka mahakamani, inashindwa nini kukamata watu wanaowaua wanaoikosoa.
Presentational grey line
"Ninaandika kwenye ukurasa wangu kwa mara ya kwanza baada ya miezi minne tangu Oktoba 2017. Ninamshukuru Mungu na Wasamaria wema kwa kunisaidia na kuiokoa maisha yangu kutoka kwa mikono ya 'watu wasiojulikana' Tanzania
Presentational grey line
Sammy: Wewe ulifanya nini, ulisema nini, uliandika nini hata hawa unaowashutumu kutaka kukutoa uhai kukufuata?
Ngurumo: Nimekuwa naandika kwenye magazeti kwa zaidi ya miaka 20 lakini kwa miaka kama 15, nimekuwa na makala ya maswali magumu imekuwa inawauma sana na kuwakera watawala. Utawala uliopita ulikuwa pamoja na kuchukia, ulikuwa unavumilia na wakati mwingine kufanyia kazi, lakini utawala ulioingia umekuwa hautaki kuguswa wala kukosolewa.
Sammy: Lakini Bwana Ngurumo, haya unayoyasema wewe si mwandishi pekee ambaye umekosoa serikali,kuna waandishi wengi na hata viongozi wa dini na watu wengine wamekuwa wakikosoa vitendo hivi kwa nini wakufuate wewe tu?
Ngurumo: Hilo swali waulize wao lakini wameshapotea wengi kabla yangu , tofauti yangu na wengine ni kuwa mimi ni mepata bahati tu ya kutonywa.
Serikali yasemaje kuhusu shutma hizo?
Serikali ya Tanzania nayo imekanusha madai hayo, mwandishi wetu Sammy alizungumza na Dk. Hassan Abbas ambaye ni msemaji wa serikali ya Tanzania. Haya hapa ni mazungumzo yao:
Sammy :Bwana Ngurumo anaishutumu serikali kutaka kutoa uhai wake kwa sababu ya kazi yake unalizungumziaje
Dk.Abbas: Mimi niseme kuwa madai yake hayana msingi na labda ana ajenda zake ambazo nafikiri tusubiri kuziona kwa sababu serikali ya Tanzania imesajili vyombo vingi vya habari na ndio inayoruhusu mwanahabari kufanya kazi zake na kila mwanahabari anatekeleza kazi zake kwa misingi ya taaluma
Dk Hassan AbbasHaki miliki ya pichaTWITTER
Image captionDk Hassan Abbas
Sammy: Anatoa mifano ya watu wamepotea, kwa sababu za kisiasa, anaamini kuwa kuna watu wanakamatwa, na yeye kwa kuwa amekuwa akikosoa serikali kwa muda mrefu ndio sababu anadai serikali inataka kutoa uhai wake?
Dk.Abbas: Mimi nafikiri Ngurumo tumsaidie, watu wanaodai kuwa mtu fulani amechukuliwa hatua kwa sababu ya kazi yake au kukosoa, nafikiri hawaitendei haki nchi, hakuna sheria ya nchi hii inayounda kosa la kukosoa serikali.
Presentational grey line

Visa vya mauaji ya kutoweka kwa watu Tanzania

  • Mauaji ya Kibiti mwaka 2017: Viongozi wa CCM, askari zaidi ya 10 na wananchi karibu 40 katika eneo la Kibiti walishambuliwa na kuuawa na watu wasiojulikana.
  • 11 Februari, 2018 Kiongozi wa Chadema Daniel John alitekwa na kisha aliuwawa kikatili wakati wa Kampeni za Uchaguzi mdogo wa jimbo la Kinondoni. Mwili wake ulipatikana mnamo 14 Februari.
  • Mnamo 7 Septemba, 2017, Mnadhimu Mkuu wa upinzani bungeni, mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu alipigwa risasi na watu wasiojulikana katika eneo la Area D Mkoani Dodoma. Bw Lissu pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika.
  • 21 Novemba, 2017 Mwandishi wa habari wa Mwananchi Communications Limited Azory Gwanda alipotea katika mazingira ya kutatanisha na mpaka sasa hajapatikana.
  • Msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema Ben Saanane alipotea katika mazingira ya kutatanisha.
Presentational grey line
Sammy:Kwa hiyo unahakikishia watu kuwa uhuru wa kujieleza na habari tanzania uko safi kabisa?
Dk.Abbas:Uko salama kwa mujibu wa vigezo vya kisheria, kwamba waandishi wa habari wanafanya kazi yao kwa hiyo nafikiri Tanzania tuko salama tunaendelea vizuri, niwaambie wana habari watimize wajibu wao wasitengenezewe hofu isiyokuwepo lakini kikubwa tunazo sheria na taratibu za taaluma yetu.
Kuhusisha suala la Azory kutekwa au kupotea na serikali; tujiulize suala moja, Azory ameandika kitu gani cha kukosoa kikaiudhi serikali?
Maendeleo makubwa ambayo tunafanya kwenye nchi yetu hayawezi kuwapendeza wengi kwa hiyo tunajua wako watu watapika mambo mengi kisiasa lakini sisi tunasimama kuzingatia misingi ya sheria za nchi .
Tukitoa mfano wa Sugu, alisimama mahakamani akajitetea akachukuliwa hatua, ukitoa mfano wa Azory aliandika nini na wapi dhidi ya serikali mpaka kukawa na kiashiria kama hicho? mimi nafikiri tunahusisha matukio fulani ambayo hayana uhusiano na serikali.
Sammy: hili suala la uhuru wa kutoa habari, kupokea na kujieleza limezungumzwa na makundi mengi, asasi za kiraia,jumuia ya kimataifa na hivi karibuni waraka wa maaskofu imeelezwa kumekuwa na uminyaji uhuru wa kujieleza kutoa maoni yao kwa ujumla , wanauliza kwa nini Tanzania imefikia hatua hii?
Dk.Abbas:Mjadala wa uhuru wa kujieleza uko sehemu zote duniani ,mjadala kuhusu weledi wa waandishi wa habari na usahihi wa habari zinazotolewa, unaposema haki ya kupata habari si habari zozote, bali habari sahihi, na kuna misingi ya kufuata. misingi yakitaaluma isipofuatwa kuna hatua za kisheria zitachukuliwa.Ukimdhalilisha mtu ukichukuliwa hatua huwezi kusema ni kukiuka uhuru wa habari .Ukiingilia usalama wa taifa nchi zote duniani zinalinda usalama wake ukiingilia unachukuliwa hatua.

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post