Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma amepewa saa 48 kujiuzulu, wadhfa wake huo.
Kwa mujibu shirika la Utangazaji la Afrika Kusini -SABC- na vyanzo vingine vya habari, hatua hii inakuja baada ya mlolongo wa mazungumzo yaliyofanywa na chama tawala cha nchini humo ANC.
Duru zinasema ANC kilifanya mazungumzo marefu baadaye kuwatuma watu wawili nyumbani kwa Rais Zuma jijini Pretoria kwenda kumfikishia ujumbe wa chama ana kwa ana ya kwamba Zuma ajiuzulu mwenyewe au chama kimng'oe madarakani.
Lakini haijulikani bado kwamba Rais Zuma alipokeaje ujumbe huo.
Hatua hii ya ANC inaonekana ndio njia rahisi zaidi ya chama hicho kumng'oa rais Zuma madarakani badala ya kusubiri utaratibu wa bunge ambao ungeweza kuwa mrefu na wenye madhara zaidi kwa chama cha ANC.
Rais Jacob Zuma ambaye anakabiliwa na mashtaka kadhaa ya rushwa, alishindwa uongozi wa chama tawala Desemba mwaka jana.
Kiongozi mpya wa ANC, Cyril Ramaphosa anaongoza shinikizo za kumuondoa Zuma katika nafasi yake hiyo ya Urais, na hatimaye kushika pia nafasi hiyo.
Ramaphosa ameahidi pia kupambana na rushwa iliyokithiri na kukijenga upya chama cha ANC, wakati nchi hiyo ikielekea katika uchaguzi mwakani.