Mtulia Achaguliwa kwa Kukosa Kura za Watu 40,000 wa Mwaka 2015 Kinondoni


Wakati Maulid Mtulia wa CCM akitangazwa mshindi wa ubunge katika Jimbo la Kinondoni, takwimu zinaonyesha kuwa amechaguliwa na chini ya nusu ya wapiga kura waliomchagua mwaka 2015.

Hali hii ni tofauti kwa Dk Godwin Mollel wa CCM, ambaye alitangazwa mshindi katika Jimbo la Siha kwa kupata kura 25,611 ikiwa ni zaidi kwa kura 2,865 ya zile alizopata mwaka 2015 ambazo ni 22,746.

Katika matokeo yaliyotangazwa jana na msimamizi wa uchaguzi wa Kinondoni, Aaron Kagurumjuli, Mtulia ameibuka mshindi kwa kupata kura 30,247 huku Salum Mwalimu wa Chadema akipata kura 12,353.

Kagurumjuli ambaye pia ni mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Kinondoni alisema idadi ya wapiga kura walioandikishwa walikuwa 264,055, waliopiga kura ni 45,454 sawa na asilimia 17.2, kura halali ni 44,867 na zilizoharibika ni 587.

Idadi hiyo ya kura za Mtulia ni nusu ya zile alizopata mwaka 2015 katika Uchaguzi Mkuu akiwa CUF na kuungwa mkono na vyama vinavyounda umoja wa Ukawa kwani alipata kura 70,337 dhidi ya mpinzani wake wa CCM, Idd Azzan aliyepata kura 65,964.

Bila kujali sababu nyingine, hii ina maana kuwa watu 40,000 ambao walimchagua Mtulia mwaka 2015 hawakujitokeza au hawakumchagua juzi.

Matokeo ya Mtulia ni tofauti na yale ya Siha ambako msimamizi wa uchaguzi, Valerian Juwal alimtangaza Dk Mollel mshindi kwa kupata kura 25,611 huku Elvis Mosi wa Chadema akipata kura 5,905.

Kwa matokeo hayo, Dk Mollel aliyehama Chadema na kujiunga na CCM amepata kura zaidi ya zile za mwaka 2015 ambazo ni 22,746 zilizompa ushindi dhidi ya Aggrey Mwanri wa CCM aliyekuwa akitetea jimbo hilo aliyepata kura 18,584.

Akizungumzia matokeo hayo, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Katoliki Ruaha (Ruco), Profesa Gaundence Mpangala alisema chaguzi ndogo za ubunge hujitokeza kwa mtu kufariki dunia au mahakama kutengua ushindi lakini hili la watu kujiuzulu na kugombea tena ni kitu kipya.

“Wananchi wamechoka na siasa za aina hii mpya ya mtu kujiuzulu na huyohuyo anagombea tena, huu ni mgomo baridi ambao ili kuumaliza tuondokane na siasa za aina hii,” alisema Profesa Mpangala.

Alisema mwanasiasa kuwa upinzani au chama tawala si kosa; kubwa ni kuleta maendeleo kwa wananchi na kila upande haupaswi kuuona mwingine ni adui.

“Rais wa sasa wa Zimbabwe (Emmerson Mnangagwa) ameamua kukutana na vyama vyote vya upinzani ili kujadili jinsi ya kuendesha uchaguzi huru na haki ujao, sijui hapa Rais (John) Magufuli anaweza kukutana na wapinzani, sioni hilo,” alisema.

Akichambua matokeo hayo kwa jumla, Profesa Benson Bana wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema, “Unajua chaguzi ndogo hazijalishi zinasababishwa na kifo au mahakama lakini zimekuwa hazina mvuto na kwa mfumo wetu wengi wape ndicho kinachojitokeza.”

Alisema hakuna sababu za msingi zinazomlazimisha mtu kwenda kupiga kura na wengine wanaona hata wasipokwenda kupiga kura hakuna tatizo au wanajiuliza mbunge atamsaidia kitu gani.

    

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post