Odinga atarajiwa kuapishwa leo na upinzani Kenya


Hali ya wasiwasi imetanda nchini Kenya leo Jumanne, baada ya kiongozi mkuu wa upinzani nchini humo Bwana Raila Odinga, kushikilia kuwa ataapishwa leo kama rais wa nchi hiyo.

Muungano wa upinzani National Super Alliance (Nasa) umesema hafla hiyo itafanyika katika uwanja wa Uhuru Park, Nairobi. Baada ya sherehe hizo kuahirishwa mwezi uliopita, muungano mkuu wa upinzani nchini humo-NASA, bado unaendelea na msimamo wake wa kuwaapisha viongozi wake Raila Odinga na Stephen Kalonzo Musyoka, kama Rais na Makamu wa rais wa Jamhuri ya Kenya.

Idara ya Polisi nchini humo tayari imepiga marufuku shughulihiyo na kuwatahadharisha wote ambao wanapanga kushiriki.

Mwanasheria Mkuu Prof Githu Muigai mwishoni mwa mwaka jana alisema mpango wa kumuapisha Bw Odinga ni sawa na uhaini wa kiwango cha juu.

Inakisiwa kuwa idadi kubwa ya wafuasi wa upinzani, wamesafiri usiku kucha kutoka maeneo ya mbali ili kufika Nairobi kwa sherehe hizo.

Agosti 2017, uchaguzi ulipofanyika, tume ya uchaguzi ilitangaza kwamba alikuwa ameshindwa na Rais Kenyatta.

Kiongozi huyo wa upinzani alipinga matokeo hayo Mahakama ya Juu na uchaguzi huo ukafutiliwa mbali na uchaguzi mpya kuandaliwa tarehe 26 Oktoba.

Maafisa wa polisi wakiwa na magari ya kukabiliana na gharia karibu na uwanja wa Uhuru Park mapema leo

Lakini Bw Odinga alisusia uchaguzi huo akisisitiza kwamba mageuzi yalihitajika katika tume ya uchaguzi kabla ya uchaguzi huru na wa haki kufanyika.

Uchaguzi wa marudio ulifanyika, ingawa shughuli hiyo ilitatizwa ngome za upinzani, na Bw Kenyatta akapata ushindi mkubwa.

Mahakama ya Juu iliidhinisha kuchaguliwa kwa Bw Kenyatta na baadaye akaapishwa tarehe 28 Novemba, Bw Odinga alisema kamwe kwamba hatamtambua kama kiongozi aliyechaguliwa na wananchi Kenya.

Maafisa wa vikosi mbalimbali vya kulinda usalama wamekuwa wakishika doria uwanja wa Uhuru Park na maeneo mengine ya mji.

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post