Leo January 10, 2018 Mahakama ya Wilaya ya Ilala imeshindwa kusoma hukumu ya kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha inayomkabili Salum Njwete ‘Scorpion’ kwa sababu Hakimu hajamaliza kuandaa hukumu hiyo.
Hukumu hiyo ilitarajiwa kusomwa leo na Hakimu Mkazi, Flora Haule lakini aliuambia upande wa mashtaka na utetezi kuwa bado hajamaliza kuandaa hukumu ya kesi hiyo.
Baada ya kueleza hayo, Hakimu Haule aliahirisha kesi hiyo hadi January 22, 2018 kwa ajili ya kusoma hukumu hiyo.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Njwete anayetetewa na wakili Juma Nassoro anaidaiwa September 6, 2016 saa 4 usiku maeneo ya Buguruni Dar es Salaam, aliiba cheni ya Silva yenye uzito wa gramu 34 ikiwa na thamani ya Sh 60,000, simu ya mkononi na fedha Sh. 330,000 vyote vikiwa na thamani ya Sh 474,000 mali ya Said Mrisho Said.
Pia anadaiwa kabla na baada ya kutekeleza tukio hilo, Scorpion alimchoma Mrisho sehemu mbalimbali za mwili wake ikiwemo machoni, tumboni na mabegani ili kurahisisha kupata mali hizo.
Tags
kitaifa