Kesi
ya kutakatisha Dola za Marekani 375,418 inayomkabili aliyekuwa Rais wa
shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi na wenzake, imepigwa
kalenda hadi Januari 11, 2018 baada ya upande wa Jamhuri kudai bado
haujakamilika.
Hata
hivyo, upande wa utetezi uliiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,
Dar es Salaam, kuuamuru upande wa mashtaka kuharakisha upelelezi wa kesi
hiyo.
Kesi hiyo ilitajwa jana na Hakimu Mkazi Mkuu Wilbard Mashauri.
Wakili
wa Serikali Mwandamizi, Leonard Swai, alidai kuwa upelelezi bado
haujakamilika, hivyo akaomba tarehe nyingine ya kutajwa.
Wakili
wa utetezi, Nehemiah Nkoko, alidai kuwa kesi hiyo ni ya muda mrefu na
kila siku wanaambiwa jalada bado lipo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Hakimu Mashauri alisema mahakama hiyo inafanya kazi ya kutafsiri sheria na kama itafanya vinginevyo itakuwa nje ya sheria.
Alisema kesi hiyo itatajwa Januari 11, 2018 na washtakiwa wataendelea kukaa mahabusu.
Washtakiwa
wengine katika kesi hiyo ni Katibu wa TFF, Mwesigwa Selestine na
Mhasibu wa shirikisho hilo, Nsiande Mwanga ambao wanakabiliwa na
mashtaka 28, ikiwamo ya utakatishaji fedha ambazo ni Dola za Marekani,
375,418.
Tags
Michezo