Jeshi la Polisi latoa Onyo

Jeshi la Polisi Kanda Maalum jijini Dar es salaam, limewaonya na kuwatahadharisha watu wenye tabia za uhalifu kutovunja sheria katika siku hizi za sikuu, kwani limekaa macho na kujipanga kuwadhibiti.
Taarifa hiyo imetolewa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es salaam Lazaro Mambosasa alipokuwa akizungumza na mwandishi wa East Africa Television, ambapo amesema kwamba hapo kesho jiji litazingirwa na askari wa kutosha kuhakikisha wakazi wake wanakuwa salama dhidi ya vitendo viovu.
"Kwanza nimepiga marufuku disco toto kwa ajili ya usalama, lakini pia kwenye fukwe polisi watakuwepo kuangalia usalama, wale wanaovizia mikoba na vitu vingine niwaambie tu hawatakuwa salama, kwani askari wetu wamejipanga kukabiliana nao, kutakuwa na ulinzi wa kutosha, askari wa jeshi la polisi, tumeomba ushirikiano kutoka kwa askari wa makampuni binafsi, walinzi shirikishi, hivyo hawataweza kwenda hatua tatu bila kudakwa", amesema Mambosasa.
Sambamba na hilo Kamanda Mambo sasa amewataka wananchi kusherehekea sikukuu hizo kwa amani wakiwa majumbani kwao na familia zao, ili kuhakikisha watoto wanakuwa salama, huku akiwaonya wale watumia vyombo vya moto kuwa makini na kufuata sheria za barabara.
"Tunaelekeza watu watii sheria, tunajua watu wakishakunywa wanapoteza ufahamu, wito ni kwamba watii sheria za barabarani na washerehekee na familia zao majumbani mwao, ili watoto waendelee kuwa salama, wasiwaache wenyewe", amesema Kamanda Mambosasa.
Kamanda Mambosasa amesema ulinzi huo mkubwa na wa hali juu utaendelea mpaka sikukuu za mwaka mpya, ili kudhibiti matukio ya uhalifu yanayotokea siku za sikukuu.

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post