Spika wa Bunge, Job Ndugai amewapa rungu wabunge wa CCM akiwataka wafunguke wakati wa mijadala na si kusimama na kupongeza tu.
Spika
alitoa kauli hiyo jana wakati wa kujadili mapendekezo ya mpango wa
maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2018/19 na mwongozo wa maandalizi ya mpango
na bajeti kwa mwaka 2018/19.
Kauli
ya Spika ilitokana na mchango wa Peter Serukamba (Kigoma Kaskazini
–CCM) ambao kwa kiasi kikubwa ulionyesha namna hali ya uchumi si nzuri
na kutoa takwimu zinazoonyesha kushuka kwa uchumi nchini.
“Katiba
iliweka utaratibu kwamba mipango ya nchi itapita hapa kwanza ninyi
muijadili. Halikuwekwa hivyo kwa bahati mbaya. Liliwekwa hivyo ili
nyinyi mseme kwa niaba ya wananchi,” alisema Spika.
Alisema,
“Katika mambo ya msingi kama haya fungukeni. Msijifunge funge hapo ooh
mimi CCM. CCM haitaki mipango mibovu. Ni wakati wenu wa kusema tumsaidie
waziri na tuisaidie Serikali ili tusonge mbele.”
Huku
akipigiwa makofi na wabunge wa upinzani na wale wa CCM, Spika alisema
“Na unapoomba nafasi ya kusema hapa uwe umejiandaa. Si ile tu naunga
mkono nafanya hivi unakaa chini”.
Wabunge
wawili wa CCM, Hussein Bashe wa Nzega na Serukamba jana walivaa ujasiri
na kueleza waziwazi kuwa uchumi uko hatarini kuporomoka, huku Kiongozi
wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe yeye alienda mbali na
kudai Serikali inatoa taarifa za uongo, akisisitiza uchumi hautajengwa
kwa mtutu wa bunduki, ubabe na vitisho.
Katika
mchango wake, Serukamba ambaye alionekana kama kuwafungulia njia
wabunge wa CCM, alisema mipango yote mitatu ni kama imeigizwa akitumia
neno la ‘copy and Paste’.
“Ukipitia
yote wamebadilisha lugha lakini kinachosemwa ni kilekile. Deni la Taifa
linapanda kwa Sh4 trilioni kwa mwaka. Maana yake tumeamua kama Serikali
kila kitu kinafanywa na Serikali,” alisema.
“Hatuwezi
kuendelea. Halipo Taifa duniani ambalo kila kitu wanajenga kwa fedha za
Serikali. Tumekwenda Moscow uwanja wa ndege wa kimataifa umejengwa na
mtu binafsi.”
Serukamba
alisema Serikali inasema inatekeleza miradi kwa ubia na sekta binafsi
(PPP), lakini katika kitabu cha waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip
Mpango hakuna mradi ulioonyeshwa.
“Serikali
hii haiamini katika sekta binafsi. Nataka Bunge hili tukubaliane Waziri
wa Fedha atuambie, Serikali hii haikubaliani na Sekta binafsi. Kama
tumerudi kwenye ujamaa tuambiane,” alisema.
“Namuonea
huruma sana Rais. Anahangaika lakini wenzake hawamwambii ukweli. Humu
ndani waziri anaongelea kukusanya kodi peke yake. Tunakusanya kodi kwa
nani?”
“Leo
mabenki yanakufa. Mabenki yote yanaonyesha kushuka kwa faida. Hata
mabenki makubwa. Hata uchumi unaofanya vizuri tunaangalia ufanisi wa
sekta ya mabenki na ufanisi wa soko la mitaji”
“Nchi
ni yetu sote. Haiwezekani viwanja vya ndege tujenge kwa pesa zetu, reli
tujenge kwa pesa zetu, umeme pesa zetu, barabara kwa pesa zetu sisi ni
nani. Dunia yote imeenda kwenye sekta binafsi”
“Leo
ukienda kwenye mabeki kila kitu kimeshuka. Personal lending (mikopo kwa
wafanyakazi) mwaka 2015 ilikuwa asilimia 25.5 leo ni asilimia 8. Mikopo
ya biashara mwaka 2015 ilifika asilimia 24.6 leo ni asilimia tisa 9.”
“Hakuna
anayesema na tukisema utaanza kupewa majina. Mambo hayako sahihi kwa
sababu moja tu, mpango wetu wa mwaka huu ndiyo wa mwaka jana na ndio wa
mwaka juzi,” alisisitiza Serukamba.
Akizungumzia
hilo, Bashe alisema vigezo vya kupima uchumi wowote duniani una kioo na
kioo cha uchumi wowote unaokua au kusinyaa au unaoshuka ni taasisi za
fedha, biashara na soko la mitaji.
Alisema
mikopo kwa watu binafsi imeshuka hadi asilimia 8.9 mwaka huu kutoka
asilimia 25 za mwaka 2015 huku mikopo ya kibiashara nayo ikishuka hadi
asilimia tisa kutoka 24 za mwaka 2015.
“Na
maneno haya siyatoi pengine ni report za BoT (Benki Kuu ya Tanzania)
inayoishia Juni mwaka huu. Kilimo leo ni negative 9 (hasi) kutoka
asilimia sita. Manufacturing kutoka asilimia 30 hadi tatu,” alisema.
“Uchumi
wetu unasemwa unakua kwa asilimia 6.8 lakini taarifa ya mwisho
niliyonayo inasema asilimia 5.7,” alisema Bashe huku akisisitiza kuwa
Serikali haijajipanga katika kutekeleza mpango huo.
“Waziri
katika kitabu chake hiki anasema watafanya uhimilishaji wa mifugo
459,000 na tunapanga kuzalisha hay (majani ya ng’ombe) 445,000 kitakwimu
hay moja ina uzito wa kilo 25”.
“Chakula
hiki ukikigawa kwa siku 365 kinalisha ng’ombe 1,600 tu. Huku unapanga
kuzalisha ng’ombe 400,000 lakini unaandaa chakula cha kulisha ng’ombe
1,600?”alihoji Bashe.
Alisema
mapinduzi ya viwanda hayawezekani bila kuwekeza katika sekta ya kilimo
na kwamba, Serikali inajaribu kudhibiti mfumuko wa bei kwa kuwatia
umasikini wakulima.
“Yaani
tunadhibiti mfumuko wa bei kwa kumtia umasikini mkulima. Aina gani za
economy (uchumi) hizi? Waziri amejikita kwenye kodi tu badala ya
kujikita kwenye uzalishaji,” alisema.
Bashe
alisema katika kitabu chake, waziri Mpango ameeleza namna miradi
itakavyofaliwa kuwa ni pamoja na kuboresha mashine za kielektroniki
(EFD) na kuanzisha maabara ya TRA.
“Haumsikii
akisema tutawekeza bilioni moja kwenye kilimo cha mahindi ili tuweze
kupata. Huwezi kukamua maziwa ng’ombe usiyemlisha,” alisema Bashe.
Alisema,
“VAT (Kodi ya Ongezeko la Thamani) na PAYE (lipa kadri unavyopata)
zimeshuka yeye anasema ni kwa sababu kampuni zimepunguza wafanyakazi.”
Bashe
alisema katika kamati ya bajeti walimshauri Waziri Mpango kutoongeza
kodi katika viwanda vya bia na vinywaji baridi kwa vile ingepunguza
uwezo wa uzalishaji lakini hakuwasikiliza.
Akichangia
katika hilo, Mbowe aliwapongeza Serukamba na Bashe kwa kuwa wa kweli na
kueleza kuwa wabunge hawataisaidia nchi kama watakuwa wanafiki na
kusema wataisaidia kwa kuikosoa pale inapofaa kuikosoa.
“Tutaisaidia
nchi hii kwa kuwa wa kweli na kukosoa katika mambo ambayo ni lazima.
Tupongeze pale panapostahili. Tusipoikemea Serikali na kuiambia ukweli,”
alisema.
Mbowe
alisema, “Kwamba wale wanaosema ukweli wanastahili kufa, wale
wanaoikosoa Serikali wanastahili kuumizwa hatutafika. Chama chochote cha
siasa kikifikia mahali pa kutotaka ushauri lazima kife.”
“Maumivu
yanapotokea kwa wananchi ninyi CCM ndio mnawajibika kuanzia Rais,
mawaziri na wabunge wa CCM. Ninachoona kinafanyika kwa juhudi sana ni
kuirudisha nchi kwenye Ujamaa,” alisema Mbowe.
Alisema,
“Mahusiano kati ya Serikali na Sekta binafsi sio mazuri. Hatutajenga
uchumi wa nchi hii kwa mtutu wa bunduki. Hatujengi uchumi wa nchi hii
kwa ubabe na vitisho. Ni lazima Serikali itambue kuwa sekta binafsi ndio
injini ya uchumi na serikali ni bodi. Hakuna taifa lolote limeendelea
duniani kwa kuipuuza sekta binafsi.”
Alisema,
“Hakuna Taifa lolote duniani liliendelea kwa kufikiria sekta binafsi ni
wezi. Kufanya biashara nchini hii chini ya awamu ya tano ni kiama.
Wafanyabiashara wote wa ndani na nje wanalia.”
“Leo
Rais anahimiza viwanda ili mwaka 2025 iwe nchi yenye uchumi wa kati.
Huwezi kujenga viwanda kwa kutegemea soko lako la ndani ni lazima
utegemee masoko ya nchi jirani. Lazima tufungue mipaka Lakini ukitizama
mahusiano yetu na nchi za Afrika Mashariki tunafunga mipaka. Tunachoma
vifaranga, tunapiga mnada ng’ombe za watu,” alisema.
“Kuna
suala la utawala bora. Ukizungumza na kuchambua uchumi leo unashitakiwa
. Sisi wapinzani tufanye nini? Serikali inatoa takwimu za uongo. BoT
inatoa takwimu zinazotofautiana na za wizara”
“Kama
tusipojipa ujasiri wa kuikosoa Serikali pale inapobidi, msiba
utatuumbua. Hali yetu ya uchumi ni ngumu. Uchumi si Fly Over au
Bambadier sita. Uchumi ni kipato kwa wananchi wa kawaida,” alisema
Mbowe.
“Watanzania
wanazidi kuwa masikini na kundi dogo ndio linaona kukua kwa uchumi wa
taifa. Kukua kwa uchumi tunakoambiwa hakuoani na maisha ya watanzania.
Watanzania wanazidi kuwa masikini”
Hata
hivyo, katika mchango wake, Mbunge wa Sumve (CCM), Richard Ndassa
alimtaka waziri Mpango kuacha tabia yake ya kiburi (arrogance) kwa vile
tabia hiyo haisaidii Serikali.
“Sina
uhakika hata kama simu za wabunge unapokea. Jitahidi kusikiliza kamati
za bajeti. Ukiendelea hivyo iko siku utakwama na utakaporudi kwetu na
sisi hatutakusikiliza,” alisema.
“Wewe
si msikivu kwa wabunge. Jaribu kubadilika sisi wote tuko kwenye boti
moja na hakuna ambaye anataka kutoboa boti. Sisi ni wabunge wenzako.
Sikiliza ushauri,”.
Mjadala
huo utaendelea hadi Jumatatu ijayo na baadaye Bunge litaingia katika
kupokea miswada mbalimbali ukiwamo muswada wa kuanzisha Wakala wa Meli
Tanzania wa mwaka 2017.
Tags
Siasa