Manchester United wameshinda fainali ya Kombe la Europa kwa kuifunga Ajax Amsterdam kwa mabao 2-0 mjini Stockholm Sweden.
Mapema kabla ya mchezo huo kuanza, timu hizo mbili zilitoa heshima zao kwa watu waliopoteza maisha katika shambulio mjini Manchester. Pia wachezaji wa Manchester United walivaa vitambaa vyeusi mikononi kama ishara ya heshima kwa waathirika.
Wakicheza bila ya mfungaji bora wao Zlatan Ibrahimovic, pamoja na mabeki Marcos Rojo, na Luke Shaw, pamoja na Erick Bailly anayetumikia adhabu ya kadi nyekundu, kikosi cha Mourinho kililazimika kujituma kwenye mchezo huu wa 64 msimu huu.
Wakitumia uzoefu, pamoja na jinsi walivyojipanga, waliweza kukisumbua kikosi cha Ajax ambacho kilikuwa na wachezaji chipukizi, wakiwa na wastani wa umri wa miaka 22.
Manchester United sasa wanaungana na Chelsea, Tottenahm na Manchester City katika kucheza Klabu Bingwa Ulaya. Pia ushindi huu utawaingizia kitita cha takriban pauni milioni 50.
Hili ni kombe la Pili Mourinho anashinda na United katika msimu wake wa kwanza. United walishinda Kombe la Ligi mwezi Februari.