Unashindwa Kuweka Akiba Ya Kipato Chako Kidogo? Tumia Njia Hizi..!!!


“Kweli natafuta na napata… lakini fedha hazitoshi kabisa…”. Hizo ni kawaida kuzisikia kauli hizi katika maisha ya kila siku ya watanzania wengi hususan huku uswahilini kwetu ambapo wengi tunafanya kazi za kipato cha chini.

Ingawa kuweka akiba ni mtihani mkubwa kwa watanzania wengi, lakini ni mtihani mgumu zaidi kwa wananchi wa kipato cha chini ambao maisha yao yanategemea sana kile wanachokipata, lakini hata wanapokipata huwa hakitoshi siku zote.

Kwa bahati mbaya utamaduni wa kuweka akiba kwa wananchi wengi nchini ni utamaduni mgumu kuuishi, hii inatokana na mtazamo wa wengi kuwa akiba ni fedha inayowekwa kutokana na ‘ziada katika kipato’ cha mtu fulani. Mtazamo huo ni kikwazo kikuu cha kwanza, kwa kuwa kama unataka kuweka akiba lazima ujenge tabia ambayo baadae itakuwa utamaduni wako (mtindo wa maisha) wa kuweka akiba.

Tunapaswa kufahamu kuwa kipato kinachoitwa cha ‘ziada’ hakina maana ya kuwa ‘kimezidi’, hivyo kutokuwa na pato la ziada kwenye pato kuu kisiwe kigezo cha kwanza cha kutoweka akiba. Lakini hili halitawezekana kama hautajenga utamaduni wa kuweka akiba na kuuishi utamaduni huo.  Yaani kuweka akiba kuwe sehemu ya maisha yako.

Ni muhimu sana kuweka akiba, hiyo nilijifunza kutoka kwa bibi yangu ambaye hivi sasa amepumzika (Apumzike kwa Amani), ambaye alikuwa akiweka kibubu kwa kufukia kwenye sakafu ya udongo ya nyumba yake ya nyasi. Alikuwa na kipato kidogo sana na kisichotabirika, lakini ilikubidi uwe na maelezo ya kutosha kumshawishi kukigusa kibubu chake.

Ingawa nilimuona kama bahili kwa kuwa nilikuwa najua kuna sarafu anapata kutokana na kilimo chake cha mihogo kupitia shamba lake dogo, kila alipokivunja kibubu chake tulitabasamu muda wote na kusahau machungu kwani alifanya vitu vya maendeleo na kutimiza lengo fulani.

Kwa maisha ya sasa, njia hiyo inaweza kuwa ‘kituko’ lakini unaweza kutumia njia mbadala kwa lengo lilelile.

Hii ni namna ya kujenga utamaduni wa kuishi na kuweka akiba kupitia kipato kidogo unachokipata. Kama kipato chako ni kidogo sana, ukizifuata hizi unaweza kuwa na uwezo wa kuweka akiba angalau kwa asilimia 10 ya pato lako kwa kila mwezi.

1. Kuwa na nidhamu ya fedha

Iheshimu kila sarafu unayoipata. Tengeneza bajeti yako na utafakari kwa kuweka vipaumbele vya mahitaji yako kulingana na kipato. Hakikisha hautumii fedha bila kuwa na sababu za msingi na kujiridhisha kuwa unahitaji kutumia kiasi hicho cha fedha.

Hii ndio maana ya kuwa na nidhamu katika matumizi ya fedha kwa kuwa ingawa unao uwezo wa kutumia chochote ulichonacho bila kuhojiwa, bado unaweza kutengeneza ‘bunge’ kichwani kwako na kujadili mantiki ya matumizi husika.

2. Weka Malengo yanayopimika, yategemeze na akiba yako

Ili uwe na nguvu ya kuweka akiba, unapaswa kuweka malengo muhimu unayotakiwa kuyafikia katika kipindi fulani. Hakikisha malengo hayo yanapimika na yanatekelezeka endapo utaweza kuweka akiba kwa kipindi hicho. Ukiweka lengo kubwa sana, unaweza kukata tamaa baada ya kugundua hautaweza kutekeleza bila kujitesa sana au kwa muda uliopanga.

Malengo yanayopimika yatakupa nguvu ya kuweka akiba yako ndogo kwa kuwa utakuwa unaona jinsi unavyoyasogelea malengo yako kwa kupima ongezeko la akiba husika. Kumbuka kila ongezeko katika akiba yako lina maana kubwa sana kuliko kile unachokitumia kikakwisha.

3. Jitenge na Kipato chako

Ingawa wewe ndiye msimamizi na mdhibiti wa fedha zako, unapaswa kujitenga na fedha zako na kuhakikisha kuwa unakuwa msimamizi unayezitendea haki fedha hizo. Usiishi kwa kufuata kile anachofanya mtu fulani. Kama unapenda kile anachokifanya, jaribu kutafakari, weka kwenye mpango wako, kipime na anza kukifanyia kazi.

Kumbuka kuwa fedha unazoweka akiba, usipojitenga nazo na kuzichukulia kama ni fedha unazodaiwa kwa ajili ya kukamilisha jukumu au lengo fulani muhimu, utazitumia aghalabu.

4. Jipunguzie Kipato kwa Asilimia

Kwa kipato chako kuwa kidogo hakimaanishi hupati kabisa, au ndio kipimo cha mwisho cha kipato chako. Kumbuka utatumia kulingana na kile unachoingiza. Hivyo, kuwa na utaratibu wa kujipunguzia kipato chako angalau kwa asilimia 10. Asilimia hizo uzihamishie kwenye kibubu chako cha muda mrefu cha malengo makubwa. Hata kama umechukua mkopo kwa ajili ya kitu fulani, tumia njia hii kuweka akiba. Wakati unamaliza kurejesha mkopo wako, kibubu chako kitakuwa mtaji mpya.

5. Kaa Mbali na Kibubu chako!

Kwa usili ya binadamu yoyote, tamaa ni sehemu ya maisha yetu, ila tunazidiana kiwango cha tamaa. Unapotamani kuwa na kitu fulani, mara nyingi unajiangalia mifukoni. Hivyo tamaa ya jambo fulani ikikuzidia, unaweza kujikuta ukivunja kibubu chako kabla ya muda muafaka kwa sababu tu kiko karibu na wewe.

Tafuta namna nzuri ambayo itakuwa rahisi zaidi kwako kuweka pesa hiyo lakini vigumu sana kwako kuichukua.

Kwa mfano wa kawaida tu, unaweza kufungua akaunti Benki, kisha ATM Card ukaiacha kwa mtu unaemuamini mkoa fulani, mtu huyo asifahamu ‘password yako’ lakini pia mwambie lengo lako. 
Wakati yeye hajui password ya ATM Card yako japo anayo (Hasa zile zenye picha), wewe pia unafahamu password lakini huna uwezo wa kuchukua pesa bila ATM Card yako. Ugumu huo unaweza kukusaidia wewe kwa hali ya kawaida kabisa.

Hata hivyo, hivi sasa kuna mifuko mingi ya kijamii pamoja na njia za kibenki ambazo ni salama zaidi ambazo zitakufanya kuweka pesa kwenye akaunti yako lakini huwezi kuichukua kwa muda fulani, na utakapofikisha muda muafaka unapata riba ya asilimia kadhaa.

Kumbuka usipoweka akiba huku unawaza maendeleo makubwa, ni kama unakimbiza upepo. ‘Akiba Haiozi’.

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post