Mbinu 9 za Kuacha Tabia Mbaya

Tabia mbaya zimekuwa zikiwakabili na kuwatesa watu wengi. Haipingiki kuwa tabia mbaya huwazuia watu wengi kufikia malengo yao kwenye maisha.

Tabia kama vile uvivu, ulevi, madawa ya kulevya, uzinzi, matumizi mabaya ya pesa, ugomvi, kupoteza muda, n.k. ni baadhi tu ya tabia ambazo zimekuwa zikiwaathiri watu wengi.

Hata hivyo, waathiriwa wa tabia hizi wengi hutamani kuziacha, lakini wanashindwa kufahamu waanzie wapi na watumie njia gani ili kuacha tabia hizo.

Ikiwa basi unataka kuboresha maisha yako, karibu nikufahamishe mbinu 9 unazoweza kuzitumia ili kuacha tabia mbaya.

1. Jikumbushe na tafakari madhara ya tabia hiyo
Ili kupata motisha wa kuacha tabia mbaya, kila mara jikumbushe na tafakari madhara unayoyapata kutokana na tabia hiyo.

Kwa mfano ikiwa ni tabia ya ulevi unaweza kujikumbusha madhara kama vile kupata maradhi, kifo, upotevu wa pesa, kutokuthaminika n.k. ambayo ni madhara yatokanayo na pombe.

2. Epuka watu na mazingira yanayosababisha tabia hiyo
Tabia nyingi mbaya huchangiwa na watu au mazingira fulani. Ikiwa una marafiki wanaokushawishi kuvuta madawa ya kulevya au kunywa pombe, basi waepuke.

Inawezekana pia ni mazingira yanayokushawishi kufanya matendo hayo, inakupasa pia kuepuka mazingira hayo yanayokushawishi ili uweze kuacha tabia hiyo inayokukabili.

Kumbuka! Unapokaa kwenye mazingira yanayoshawishi kufanya ngono, kulewa, kuvuta madawa ya kulevya n.k. ni vigumu kuepuka au kuacha tabia hizo.

3. Anza taratibu kuacha
Mara nyingi tabia uliyoizoea ni vigumu kuiacha kwa siku moja. Hivyo jitahidi kuiacha taratibu mpaka ipotee kabisa.

Kwa mfano kama unakunywa chupa sita za pombe kwa siku, anza kwa kujitahidi kunywa moja au mbili na hatimaye uache kabisa.

4. Jiwekee malengo
Malengo yana manufaa makubwa sana kwenye maisha au jambo lolote tunalotaka lifanikiwe. Kwa kujiwekea malengo utaweza kuwa na kitu kinachokuongoza katika mchakato mzima wa kuacha tabia mbaya inayokukabili.

Kwa mfano unaweza kujiwekea malengo ya namna hii:

Kabla ya tarehe fulani ninatakiwa niwe nimeacha kabisa tabia hii.

Tarehe fulani ninatakiwa niwe nimenunua au nimefanya kitu fulani kutokana na pesa nilizookoa kutokana na kuacha tabia hii.

Tarehe fulani ninatakiwa niwe nimepona kabisa madhara niliyoyapata kutokana na tabia hii.

Haya ni mfano tu wa malengo ambayo unaweza kujiwekea na yakakuongoza na kukuhamasisha kuacha tabia mbaya inayokukabili.

5. Jipe kazi au ratiba ngumu
“Akili isiyofanya kazi ni karakana ya shetani.”

Mara nyingi watu hutekeleza tabia mbaya pale ambapo wanakuwa wamekaa bila kazi. Binadamu anapokaa bila kazi, huufanya mwili na akili yake kujitafutia kazi nyingine ambazo kimsingi siyo nzuri.

Unapojiwekea ratiba ngumu, hutopata nafasi ya kulewa, kufanya uzinzi, umbea, uvutaji wa madawa n.k. Hakikisha unajiwekea ratiba ngumu tena itakayokuchosha ili usipate muda na nguvu za kufanya tabia ambayo siyo nzuri.

6. Jikumbushe manufaa ya kuacha tabia hiyo mbaya
Kama ilivyo kwenye kujikumbusha madhara ya tabia mbaya, kujikumbusha manufaa utakayoyapata baada ya kuacha tabia mbaya kutakuhamasisha sana.

Fikiri juu ya madhara ambayo hutoyapata tena iwapo utaweza kuacha tabia hiyo. Hakikisha unajizatiti kuacha tabia inayokukabili ili uweze kupata manufaa yatokanayo na kuacha tabia husika.

7. Tafuta msaada na ushauri
Mbinu nyingine itakayokusaidia kuacha tabia mbaya ni kwa kutafuta msaada wa ushauri kutoka kwa washauri mbalimbali. Wapo watu mbalimbali unaoweza kuwatumia kama vile wataalamu wa ushauri, wataalamu wa tiba, viongozi wa dini n.k.

Ikiwa pia kuna mtu mwingine anayetaka kuacha tabia mbaya, shirikianeni kwa pamoja ili kusaidiana kuacha. Mnaweza kushindana juu ya ni nani ameweza kuacha mapema kuliko mwingine au kuhamasishana kati ya mmoja na mwingine.

8. Waeleze watu lengo lako
Kuacha tabia mbaya ni rahisi zaidi pale unapowaeleza watu kama vile wanafamilia au marafiki zako juu ya lengo lako.

Waeleze ili wakusaidie na pia iwe ni hamasa kwako ya kuacha, kwani kwa njia hii umeshajihukumu mwenyewe kuwa unaacha tabia mbaya; hivyo kuendelea kuifanya kutakuaibisha wewe mwenyewe.

Usijitahidi kuacha tabia mbaya kwa siri, kuwaeleza watu ni hamasa na kichocheo kizuri sana kitakachokufanya uache tabia mbaya mapema.

9. Jipongeze
Mbinu nyingine ya kufanikiwa katika kuacha tabia mbaya ni kwa kujipongeza wewe mwenyewe. Unapofanikiwa kufikia lengo fulani ulilojiwekea katika mchakato wa kuacha tabia inayokukabili, basi jipongeze kwa kufanikiwa kutimiza lengo hilo.

Kwa kujipongeza utaweza kujihamasisha zaidi ili kufikia malengo megine makubwa uliyojiwekea.

Hitimisho

Kwa hakika kuacha tabia mbaya kunawezekana kabisa ikiwa utachukua maamuzi na kuweka mipango na mikakati sahihi. Kwa kutumia mbinu nilizozieleza hapo juu, naamini utaweza kuikabili tabia mbaya inayokusumbua kwa urahisi zaidi. Unaweza, weka kwenye matendo sasa nawe utaona matokeo.

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post