Kikosi cha Gor Mahia leo kinaanza rasmi safari ya kusaka ubingwa wa michuano ya KAGAME kwa kumenyama na Rayon Sports ya Rwanda mechi ikipigwa saa 8 mchana.
Gor Mahia waliwasili jana jijini Dar es Salaam na leo watakuwa Uwanja wa Taifa kuchuana vikali na wakongwe wa Ligi ya Burundi.
Kikosi cha Gor Mahia FC chini ya Kocha Dylan Kerr kitakuwa kinacheza mchezo huo bila ya kuwa na Mshambuliaji wake hatari, Meddie Kagere ambaye amejiunga na Simba SC kwa kusaini mkataba wa miaka miwili.
Mbali na kukosekana kwa Kagere, Gor Mahia wametamba kuwa bado wataendelea kufanya vizuri kutokana na kuwa na wachezaji wengine ambao wataziba nafasi ya kutokuwepo kwake.
Mechi zingine ambazo zitapigwa leo ni JKU ya Zanzibar itakuwa inacheza kibarua chake cha pili dhidi ya Kator kutoka Sudani Kusini majira ya saa 1o jioni kwenye Uwanja wa Chamaz Complex.
Baada ya kibarua hicho, Azam FC nao watakuwa wanacheza na Vipers SC ya Uganda kuanzia saa 1 jioni kwenye Uwanja wao wa nyumbani, Chamazi Complex.