Manahodha wa Australia, Denmark na Ufaransa wamewasilisha ombi la pamoja kwa shirikisho la soka duniani Fifa kulitaka liondoe marufuku dhidi ya mchezaji Paolo Guerrero.
Guerrero ni nahodha wa timu ya taifa ya Peru ambayo imepangwa kundi moja na mataifa hayo matatu.
Mnaahodha hao wanaomba aruhusiwe kucheza katika michuano ya Kombe la Dunia nchini Urusi.
Guerrero, ambaye alipatikana na kosa la kutumia kokeni Oktoba, anasema alijipata amekunywa dawa hizo akinywa chai.
Anatumikia marufuku ya miezi 14.
Kupitia barua kwa Fifa, manahodha hao watatu wameomba kuwe na "kusitishwa kwa muda" kwa marufuku yake ndipo aweze kuchezea Peru nchini Urusi
Peru wanacheza katika Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 36.
Barua hiyo ambayo imetiwa saini na Mile Jedinak wa Australia, Simon Kjaer wa Denmark na Hugo Lloris wa Ufaransa na ilitolewa na chama cha wachezaji wa soka ya kulipwa duniani FIFPro.
Barua hiyo inaomba "huruma" na "suluhu yenye usawa na stahiki" kwa mchezaji huyo ambayo itamuwezesha Guerrero kufikia "kilele" cha uchezaji wake.
Guerrero, 34, alipatikana ametumia kokeini wakati wa mechi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia dhidi ya Argentina mnamo 6 Oktoba na akapigwa marufuku ya miezi 12 awali.
Marufuku yake ilipunguzwa hadi miezi sita na kamati ya rufaa ya Fifa lakini shirika la kukabiliana na matumizi ya dawa zilizoharamishwa michezoni (Wada) likakata rufaa uamuzi huo kwenye Mahakama ya Mizozo ya Kimichezo (Cas) ambayo ilimpiga marufuku ya miezi 14.
Peru walilaza New Zealand kwenye mechi mbili za muondoano wa kufuzu Novemba ndipo wakafuzu kwa Kombe la Dunia.
Itakuwa mara yao ya kwanza kushiriki tangu mwaka 1982.
Tags
KOMBE LA DUNIA 2018