Serikali Yaanza Kuwashughulikia Wasanii Wanaovaa Nusu UCHI....Tazama Majina ya Baadhi Yao

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza amesema kuwa, serikali inafuatilia kwa karibu wasanii wote wanaoweka picha za kukosa maadili kwenye mitandao na kuwachukulia hatua.

Shonza ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaama alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari. Agizo hilo la Naibu Waziri ni matokeo ya kauli iliyotolewa na Rais Dkt Magufuli aliyoitoa mjini Dodoma wakati akizungumza na Jumuiya ya Wazazi ya CCM. 

Rais Magufuli alivitaka vyombo husika kuwachukulia hatua wasanii hasa wa kike ambao wamekuwa wakivaa nguo zinazopelekea kumomonyoka kwa maadili.

Wakati akizungumza hayo Naibu Waziri alitaja majina ya wasanii ambao wameanza kuwachukulia hatua ambapo baadhi wametakiwa kufika ofisini kwake huku mwingine akifungiwa kujihusisha na masuala ya sanaa kwa muda wa miezi sita.

Shonza amemtaka msanii, Jane Rimoy maarufu kwa jina la Sanchi kufika ofisini kwake mara moja kutokana na kuchapisha mitandaoni picha zisizo na maadili.

Mbali na Sanchi, Shonza ametoa maagizo, ”Ninamtaka Msanii wa Bongo Fleva, Gift Stanford maarufu kama Gigy Money kufika ofisini kwangu mara moja sababu alitumiwa ujumbe lakini hakujibu, hivyo ajue kuwa hawezi kushindana na serikali.”

Pia, Naibu Waziri wa Habari, Juliana Shonza amemfungia msanii wa filamu na muziki, Suzan Michael maarufu Pretty Kind kujihusisha na shughuli zote za sanaa kwa muda wa miezi sita, kutokana na kuweka picha za utupu katika mtandao ya kijamii.

Wakati huo huo, Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Godfrey Mngereza amewasisitiza wamiliki wa studio za kutayarisha kazi za sanaa na waandaji wa kazi za sanaa (Producers) kujisajili katika ofisi za Baraza hilo. Asisitiza, kufanya kazi bila kusajiliwa ni kinyume na sheria.

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post