UNDAVA undava tu kwani Simba baada ya kuchukuliwa mchezaji wake Ibrahim Ajibu na Yanga, nayo inapambana kuhakikisha inamsajili straika Donald Ngoma wa Yanga.
Ngoma ni kama Ajibu kwani naye anaelekea ukingoni kumaliza mkataba wake na Yanga mwishoni mwa mwezi huu na bado hana uhakika wa kuongeza mkataba.
Habari kutoka ndani ya Simba, zinasema klabu hiyo imepanga kumtuma mmoja wa viongozi wake kwenda Zimbabwe kuzungumza na Ngoma ili iweze kumsajili baada ya Ajibu kwenda Yanga.
Hata hivyo, inaonekana kuna ugumu kuhusu usajili huo wa Ngoma kwani straika huyo awali amewaambia Simba kwamba anataka dau la usajili la dola 100,000 sawa na Sh milioni 219.2.
“Tunataka kupambana kumpata Ngoma lakini huyu anataka dola 100,000, hapo mshahara bado, ngoja tuone itakavyokuwa,” alisema mmoja wa watu wa usajili wa Simba.
Kutoka Yanga, habari zinasema klabu hiyo imeamua kukaa kimya kwanza juu ya Ngoma kwani inaonekana hawataweza kumlipa dola 160,000 alizotaka za usajili sawa na Sh milioni 350.8 na mshahara wa dola 14,000 kwa mwezi ambazo ni sawa na Sh milioni 30.7.
“Kwa fedha anayotaka Ngoma sidhani kama tutakuwa naye, labda atokee mwanachama mwenye fedha akazitoa bila uongozi kumgharamia,” alisema mmoja wa viongozi wa Yanga.