Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi
Kwa ufupi
Mafunzo yanalenga kuwafunda na kuwaandaa vizuri vijana wa kitanzania kimaadili, kiuzalendo na kiulinzi.
By Sharon Sauwa, Mwananchi
Dodoma. Mafunzo Jeshi la Kujenga Taifa kwa vijana wanaomaliza kidato cha sita yamewaibua wabunge bungeni leo, Jumanne baada ya Serikali kusema idadi ya vijana wanaojiunga katika mafunzo hayo imepungua.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi amebainisha kupungua kwa idadi hiyo wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Newala (CCM) George Mkuchika.
Mkuchika ametaka kujua ni asilimia ngapi ya vijana waliotakiwa kujiunga na mafunzo hayo.
Akijibu Dk Mwinyi amesema mbali na rasilimali fedha idadi hiyo imepungua kutokana na kugongana kwa tarehe za kuanza mafunzo kwa mujibu wa sheria na kufunguliwa kwa vyuo mbalimbali nchini.
Ametaja sababu nyingine ya kupungua kwa idadi hiyo ni uhaba wa miundombinu, rasilimali watu na fedha.
Dk Mwinyi alisema mwaka 2016 jumla ya wanafunzi 40,753 walimaliza kidato cha sita lakini waliojiunga na mafunzo walikuwa ni 19,990 sawa na asilimia 48.8 wakati mwaka huu wamemaliza 63,623 lakini waliojiunga ni 14,747 sawa asilimia 23.2
Mbunge wa Bukoba Vijijini (Chadema) Willfred Lwakatare ametaka kujua ni vigezo gani wanatumia katika kuteua vijana wanaokwenda katika mafunzo hayo na wasiokwenda wanawafanya nini.
Akijibu Dk Mwinyi amesema hakuna vigezo vinavyotumika katika kuwachagua vijana wanaokwenda JKT na kwamba wamekuwa wakichagua tu (randomly selection).
Naye Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Halima Bulembo amehoji kama Serikali haioni umuhimu wa kufanya mafunzo hayo yawe ya Mamlaka ya Ufundi Stadi (VET) ili vijana hao waweze kunufaika na mafunzo ya ufundi.
Akijibu Dk Mwinyi amesema kwa sasa JKT inafanya utaratibu wa kupata usajili Veta ili vyeti vya mamlaka hiyo viweze kutolewa.